Ijumaa 10 Julai 2026 - 13:42
Mwili Mtukufu wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi Wapumzishwa Katika Riwaq ya Dar al-Dhikr ya Haram Tukufu ya Imam Ridha (as)

Hawza/ Mwili mtukufu wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi pamoja na miili ya familia yake mashahidi, baada ya kufanyika kwa ibada ya mazishi, maandamano ya kuuaga na kuswaliwa Swala ya Maiti, umepumzishwa katika Riwaq ya Dar al-Dhikr, karibu na Rawdha Tukufu ya Imam Ridha (as).

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mahali hapo chini ya miguu ya Imam Ridha (as), kandokando ya kaburi Tukufu, ndilo eneo ambalo Kiongozi Shahidi kwa miaka mingi alikuwa akipita kwa unyenyekevu, khushuu na heshima kubwa ili kufanya ziara ya kubusu kizingiti cha Imam wa Huruma. Sasa mahali hapo pamegeuka kuwa makazi yake ya milele pamoja na familia yake mashahidi.

Riwaq ya Dar al-Dhikr ndani ya Haram Tukufu ya Imam Ridha (as) ndiyo mahali pa maziko ya mwili mtukufu wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi na familia yake mashahidi. Ni riwaq iliyojaa maana na ishara za kiroho; kwa wale wanaoufahamu mwenendo wa ziara, si sehemu ya kawaida tu, bali ni alama iliyo wazi ya adabu mbele ya utukufu wa Imam Mwingi wa Huruma (as).

Riwaq hiyo ipo chini ya miguu ya Imam (as), katika njia ileile ambayo Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi alikuwa akiifuata kila alipokuwa akihudhuria Haram Tukufu ya Imam Ridha (as). Aliipitia kwa uangalifu wa kiroho na mwenendo uliosheheni unyenyekevu wa hali ya juu.

Njia yake ya ziara yenyewe ilikuwa simulizi ya pekee ya unyenyekevu, simulizi ambayo sasa imepata maana maradufu kwa kusikika jina la mahali alipozikwa.

Kwa kawaida, alikuwa akiingia kupitia njia ya Dar al-Zuhd, lakini kilichoigeuza ziara zake kuwa mfano wa kudumu wa ziara yenye adabu ilikuwa ni kusimama kwake kwa hali ya kiroho katika eneo la chini ya miguu ya Imam (as). Kwake, ziara haikuwa kufika kwenye dharih peke yake, bali ilikuwa na adabu maalumu ambazo alizifuata kwa moyo wake wote.

Kabla ya jambo lolote, alikuwa akielekea kwenye Rawdha Tukufu kupitia sehemu ya chini ya miguu ya dharih tukufu, kana kwamba alitaka kwanza kusimama katika nafasi ya adabu, kisha kuomba idhini moyoni ili kuingia katika eneo la nuru. Baada ya hapo, alipitia Riwaq ya Dar al-Dhikr, akaomba idhini ya kuingia, kisha anaingia katika Riwaq ya Dar al-Surur, mahali ambapo alikuwa akisimama kwa utulivu kamili na kutulia kwa uwepo wa moyo.

Katika wakati huo, alikuwa akitamka dua kamili ya kuomba ruhusa ya kuingia (Idhn al-Dukhul), jambo ambalo kwa wasaidizi na wahudumu waliokuwa pamoja naye halikuwa tendo la kawaida la ibada tu, bali lilikuwa funzo lililo wazi kuhusu uhusiano kati ya mamlaka na utumwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kiongozi wa Umma wa Kiislamu, kabla ya kuingia katika Rawdha Tukufu, alikuwa kwanza akisimama mahali panapoashiria waziwazi adabu, unyenyekevu na maarifa ya kweli katika ziara. Na sasa, hatima imeigeuza njia hiyo hiyo aliyokuwa akiifuata daima kuwa mahali pake pa mapumziko ya milele.

Huenda kuanzia sasa, kila mja atakayepita katika njia hiyo atakumbuka kwa undani zaidi maana ya unyenyekevu mbele ya mlango wa Wilaya. Kwamba inawezekana mtu akawa katika kilele cha hadhi na utukufu, lakini bado akaanza ziara yake kutoka chini ya miguu ya Imam (as), na hatimaye naye apumzike milele katika njia hiyo hiyo chini ya kivuli cha mapenzi na rehema za Imam Ridha (as).

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha